Thursday, May 24, 2018

SOMO: NAMNA YA KUTIMIZA MAONO ULIYONAYO
Vipengele tutakavyojadili;
1. Maono ni nini?
2. Vyanzo vya maono
3. Sifa na tabia za maono
4. Mambo yatakayo kusaidia kutimiza maono
5. Mambo ya kuepuka ili yasiue maono uliyonayo
1. Maono ni nini?
i) Ni picha ya mambo yasiyoonekana machoni (mwilini/ kwenye uhalisia) bado, inayomuonesha mtu anavyotakiwa kuwa au kiwango chake halisi cha maisha- Mithali 23:7.
"Kwa maana ajionavyo mtu nafsini mwake ndivyo alivyo..."
Ni muono au ugunduzi wa maisha halisi ya mtu toka nafsini mwake!
Nafsini ni: Mahali pa akili, maamuzi na hisia.
Mtu anaweza kujua kiwango halisi cha maisha yake *kwa kuona akilini (ubongoni) mwake* kwa msaada wa Roho Mtakatifu kile apaswacho kufanya au vile atakiwavyo kuwa.
Maandiko yanasema, *"Kwa imani Musa ALIPOKUWA MTU MZIMA alikataa kuitwa mtoto wa binti Farao. AKAACHA IKULU YA FARAO NA KUJIUNGA NA WAISRAELI..."*
Huyu Musa aliweza *KUJIGUNDUA* siku moja, na *akaona maisha yake halisi* anayotakiwa kuyaishi... Alikuwa na miaka 40 wakati huo, na alishapoteza miaka 39 iliyotangulia AKIISHI MAONO YASIYO YAKE!!
Tatizo pekee la Musa alijiona nafsini mwake lakini ALIZITEGEMEA AKILI ZAKE KUWA ANAVYOJIONA (MKOMBOZI WA ISRAELI)... Matokeo yake *alifeli* na kufukuzwa Misri, akakaa Midiani miaka 40 akiwa amepoteza dira, mpaka Mungu alipomtembelea akiwa na miaka 80 kupitia kijiti kiwakacho moto!
Paulo naye ni mfano mzuri wa Maono;
Kwa miaka mingi alikuwa akiishi kama Mshika dini, akiwaua wale Mitume wa Yesu.
Lakini kuna wakati *alipojiona nafsini mwake Mungu alivyomkusudia kuwa* anasema *"aliyaona mambo yote kuwa kama mavi kwa sababu ya uzuri wa Kristo na Injili..."*
Mungu hutumia mawazo (akili na uwezo wa kuchanganua mambo yasiyokuwepo bado) kama njia ya kumsaidia mtu kujua yampasayo kufanya!
Isaya 55:8 inasema *"Mungu anawaza na mwanadamu anawaza"*
Mungu ametuumba na uwezo huu ili tuutumie kutambua *kile tunachopaswa kufanya*
Mtu akiwa amejaa Neno la Mungu na ana ushirika na Roho wa Mungu, ni rahisi sana kwa Mungu kuyatumia mawazo yake *kumuonesha yampasayo kufanya au anavyotakiwa kuwa* na haya ndiyo maono!
*aliyaona mambo yote (ambayo kabla aliyaona sahihi) kuwa ni sawa na mavi kwa sababu ya mambo sahihi aliyoyaona kutoka kwa Yesu...*
Ili neno *aliyaona mambo* maana yake kuna *uonaji* ambao ni sahihi na uonaji usio sahihi.
Uonaji sahihi ni ule wa kile ulichokiona na unakitenda au kukiishi ndicho Mungu anataka ufanye au uwe.
Na uonaji mwingine ambao unaweza kuwa unafanya kitu kizuri, watu wanakipenda au kinakubalika lakini *Mungu hana furaha nacho na hajakutuma kufanya hicho!*
ii) Maono ni mkusanyiko wa mambo ayafanyayo mtu yanayompelekea kutimiza kusudi la Mungu.
Mfano;
Kusudi langu kuu la kuumbwa ni kuwa mtu wa madhabahuni (huduma zile tano) hasa eneo la ualimu na uchungaji...
Lakini kuna mambo ambayo Mungu ameyatumia kunisogeza huku kwenye kusudi kuu.
Nyakati kwa nyakati Mungu alinipa kufanya mambo kadhaa;
Huduma za vijana
Huduma za mabinti
Akina mama
Wanaume waliooa
Kuandaa viongozi (leadership trainings)
Na mengine mengi... Na kila moja lilikuja ndani yangu na nililifanya kama *maono ya Mungu kwangu* kwa wakati na majira husika, ambayo yamenijenga kuja kuwa mimi unayenijua leo
*"Kazi kubwa ya maono ni kutimiza kusudi kuu la Mungu maishani mwa mtu"*
SHIKA SANA HII
*"Kusudi la Mungu maishani mwa mtu ndilo linalopelekea kuzaa aina ya maono ambayo akiyaishi yatampelekea kutimiza kusudi kuu alilobeba"*
USISAHAU HII
Kama Mchungaji wa ABC Kahama, mwaka huu ninapaswa kufanya kile Mungu anataka katika kipande cha kusudi nililobeba.
Na hili kutimiza hilo amenipa maono kadhaa ambayo nitayaweka kwenye matendo;
*Huduma ya wanafunzi wa sekondari*
Hii nitafundisha: umuhimu wa elimu, maadili, uongozi, kusudi, vipawa na talanta, na kujitegemea.
*Wasio na kazi*
Hawa nitawasaidia kujitambua, kuona fursa zilizowazunguka, Vipawa na talanta walizonazo, na mengine mengi yatakayobadilisha akili na mitazamo yao.
*Walevi*
Hawa nitakuwa na ofisi maalum ya kuwasaidia kuacha ulevi wa pombe, bangi, sigara, dawa za kulevya *kwa nguvu za Roho Mtakatifu!*
Hili nimelifanya tayari na kanisani kwangu nimewasaidia watu zaidi ya 30 ambao ni ushuhuda hai.
Sasa... Yote haya ni baadhi ya *maono* ambayo nitayafanyia kazi katika kutumikia kusudi la Mungu maishani mwangu (mwalimu na mchungaji), na katika kumpeleka Yesu kwa watu wengi na wa namna tofauti na kulikuza kanisa pia!
Maono yanaletwa na Mungu kutusaidia kutimiza kusudi kuu tunalokuwa tumebeba.
2. Vyanzo vya maono
Kuna vyanzo vikuu vitatu vya maono;
Mungu
Shetani
Wanadamu
Maono ya Mungu (Matendo 26:19).
Maono ya kipepo (mfano wa manabii waliooneshwa uongo na pepo, wakamtabiria Ahabu ya kuwa atashinda, lakini matokeo yake akaishia kupigwa mshale na kufa- 1Wafalme 22)
Maono ya kibinadamu
Haya yanaweza kuwa yanatokana na *kutegemea akili bila Mungu* (Mithali 3:5-7).
Au kuishi maono ya mtu mwingine;
Mfano unatoka Arusha na kuja Dar, unaona duka zuri la nguo za maharusi na unagundua Arusha hakuna nawe unakwenda unalianzisha!
Hii yote inaangukia kwenye maono ya kibinadamu.
Ni maono ya Mungu pekee ambayo yana uhakika wa kumpeleka mtu kwenye hatma yake (kutimiza kusudi kuu alilobeba)!
Mfano mzuri ni *Yusufu*, kile alichoona kwa Mungu kilimpeleka kwenye hatma yake kuu.
3. SIFA NA TABIA ZA MAONO
1. Maono ya Mungu kwa mtu huwa yanakuwa kwa mtu binafsi.
-Yusufu aliota ndoto (aliona maisha yake yajayo) akiwa peke yake.
-Musa aliona kijiti kinachoteketea akiwa peke yake
-Paulo akiwa anakwenda Dameski aliona nuru na kusikia sauti ya Bwana Yesu peke yake, wenzake wote waliokuwa naye hawakusikia wala kujua alichoambiwa na Mungu.
Point ya msingi hapa ni;
*"Maono huwa ni ya mtu mmoja... Mungu husema na mtu mmoja hata kama yatagusa maisha ya wengi au kufanikishwa na watu wengi..."*
Hivyo ni muhimu ujue haya;
1. Usikubali kukatishwa tamaa au kuambiwa haiwezekani na mtu yeyote maana *hayo maono uliyapata au kuyaona peke yako, na yako ndani yako, wewe kama unaona yanawezekana, usikubali mtu akuambie haiwezekani!*
Yusufu aliamini ndoto alizoota (maono aliyopewa na Mungu) mbali ya kupingwa na wazazi na ndugu zake.
Daudi aliamini maono yake (ya kumuua Goliati) mbali ya kupingwa na kaka zake na mfalme Sauli wakiona hawezi.
*MAONO NI YA MTU BINAFSI, USIKUBALI YEYOTE AKUAMBIE HAIWEZEKANI, KAMA UMELIONA NA UNA UHAKIKA, KOMAA SONGA MBELE*
2. Maono yoyote ya Mungu yanakuwa makubwa kuliko akili, uwezo, elimu, malighafi alivyonavyo mtu.
Daudi alikuwa mdogo kuweza kuwa Mfalme kibinadamu, ndio maana hata Samweli alishindwa kufikiria yakuwa anaweza kuwa ndo mfalme anayepaswa kumtia mafuta.
Hakuonekana kama anaweza kumuua Goliati,
Hakuonekana kama anaweza kuwaua askari 200 wa Misri na kuleta govi zao kama mahari kwa Sauli.
KILA ENEO ALIONEKANA KAMA HAWEZI AU AMEPWAYA.
Yusufu hakufanania ndoto alizoota (maono aliyobeba),
Musa hakufanania na *mkombozi wa Israeli toka utumwa wa miaka 430!*
Yesu hakufanana kwa nje na *mwokozi wa ulimwengu* ndiyo maana hakukubalika na aliitwa *mwana wa seremala!*
Maono ya Mungu kwa mtu yanakuwa makubwa kuliko yeye ili *arudi kwa Mungu pekee ili apokee nguvu na msaada wa kuweza kukamilisha hayo maono!*
Lakini pia inamsaidia mtu asiwe na kiburi au majivuno, maana hana namna ya kuweza kufanya hayo... Mwisho wa siku *Mungu pekee ndiye anayebeba utukufu!*
3. Maono yoyote ya Kimungu huanza kidogo lakini mwisho wake huwa mkubwa sana (Ayubu 8:7).
*Kila kitu kilichotokana na Mungu* huanza kikiwa kidogo.... Angalia mimea, mimba hadi uzee (ukuaji wa mtu), wanyama nakadhalika!
Yusufu alianzia mahali padogo nyumbani kwa Potifa,
Daudi alianza na kuua dubu na simba,
Musa alianza na fimbo kuwa nyoka,
Nakadhalika!!!
*Usipoanzia padogo katika maono aliyokupa Mungu, hautaenda kokote. Maono yoyote ya Kimungu huanzia padogo lakini huwa yanaishia pakubwa mno!*

1 comment: